WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Meja Jenerali Gabriel Mhidze, ahakikishe mpaka kufikia Oktoba 16, mwaka huu, dawa ziwe zimepatikana katika maeneo yote nchini.
Amesema maelekezo ya serikali ni kuwa vituo vyote vya kutolea huduma zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa, lazima zipate dawa kwa kuwa zinategemea MSD.
Agizo hilo alilitoa alipokutana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Mhidze.
“Utaratibu wa serikali ni kuwa hatutaki kuona mwananchi anaenda katika maeneo ya kutolea huduma za afya na kuelekezwa kwenda kununua dawa katika maduka ya mtaani. Serikali inapeleka fedha kila mwezi, nimetoa hii wiki, siyo Lindi tu ni pamoja na mikoa mingine yote nchini, dawa lazima ziende, kazi yenu ni kuhakikisha dawa zinakwenda kwa kuwa fedha mnalipwa,” alisisitiza
Aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema anatoa tena fedha za ujenzi, hivyo ni lazima serikali ipeleke dawa, vifaa na wataalamu.
Majaliwa aliwataka viongozi wa taasisi hiyo wahakikishe wanapeleka malori 10 ya dawa katika kila kanda, lengo ni kusaidia upatikanaji wa dawa ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Pia, Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meja Jenerali Mhidze kuhakikisha anaisimamia MSD na asisite kufanya marekebisho pale panapoonekana pana upungufu.
“Tunataka tuondoe malalamiko kwa wananchi kuhusu upatikanaji wa dawa. Fedha ipo hakuna haja ya kuwepo kwa malalamiko,” alisema.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Mhidze aliahidi kusimamia utendaji kazi wa taasisi hiyo ili kuondoa dosari zote zinazokwamisha upatikanaji wa dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma na atahakikisha upungufu huo hautajirudia.
Na MWANDISHI WETU