WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ametoa siku tatu kuanzia Novemba 15, 2021, kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu, wafuatilie njia zote za kuingiza maji katika mto huo, ambazo zimechepushwa ziwe wazi ili maji yaweze kuingia na kupunguza changamoto ya upungufu wa maji.
Pia, Majaliwa amewaagiza wasimamizi wa mabonde yote nchini wasikae maofisini na badala yake wapite katika maeneo yote wanayoyasimamia na wahakikishe yapo salama ili kuhakikisha yanakuwa na maji muda wote, pamoja na kuhakikisha wanatumia sheria iliyoanzisha mamlaka zao ili kulinda mito na maziwa.
Majaliwa alitoa maagizo hayo baada ya kutembelea vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu, kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuitaka Wizara ya Maji itafute chanzo kingine cha maji kitakachosaidiana na Mto Ruvu ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo maalumu katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi hadi washio vijijini, Wizara ya Maji hakikisheni mnatafuta vyanzo vingine ili malengo hayo yatimie.” alisema
Waziri Mkuu alieleza kuwa Mto Ruvu umeathirika na shughuli za kibinadamu zinazochangia maji kupungua, hivyo wahusika wasimamie ipasavyo ili kupunguza tatizo hilo pamoja na kusimamia idadi kubwa ya mifugo katika maeneo hayo yanayoathiri chanzo hicho.

Majaliwa pia ameziagiza Wizara za Maji, Maliasili na Utalii, na Mifugo na Uvuvi zikutane na kuona namna bora ya kuboresha mazingira ya ufugaji ili Mto Ruvu ubaki kwa ajili ya kuzalisha maji katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam pekee.
”Wizara ya Mifugo na Uvuvi nawaagiza nendeni mkazungumze na wafugaji na muweke utaratibu wa kuratibu shughuli za ufugaji bila ya kuathiri chanzo hicho cha maji. Mifugo tunaihitali lakini lazima iratibiwe,” alisema.
Alisema elimu ya ufugaji bora lazima itolewe kwa wafugaji, mfano mtu mmoja anapopeleka ng’ombe 1,000 kwenda kuwanywesha maji mtoni wanaathiri watu wengi, kwani kitendo hicho kinaathiri vyanzo vya maji na kusababisha upungufu.
Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika mitambo ya kuzalishia maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kuhakikisha wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wanapata maji ya kutosha.
“Vyanzo hivyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 520, huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 544.” alisema.

Alisema kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kwa sasa vyanzo hivyo vinazalisha lita milioni 350. Alisema ili kukabaliana na changamoto hiyo Wizara inafikiria kuwekeza katika mradi wa Mto Rufiji ambao utasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji katika mikoa hiyo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema kwa sasa hali ya uzalishaji wa maji imepungua kutoka lita milioni 520 hadi lita milioni 460 kwa siku.
Alisema kupungua huko kunatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuwepo kwa makundi makubwa ya mifugo katika eneo la chanzo cha Mto Ruvu.
“Mtambo wa Ruvu Chini ndio ambao umeathirika zaidi kutokana na changamoto ya kupungua kwa kina cha maji katika Mto Ruvu. Kwa sasa, uzalishaji umepungua kutoka lita za ujazo milioni 270 kwa siku hadi lita za ujazo milioni 119.459.”
Na Mwandishi Wetu