SERIKALI imewaagiza wakuu wa mikoa nchini kusimamia vyema utekelezaji wa uwekaji wa anwani ya makazi ili likamilike katika muda uliopangwa.
Agizo hilo lilitolewa Januari 17, 2022 na Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mfumo huo ambao unatekelezwa na serikali.
Mafunzo hayo yalifanyika kwa njia ya mkutano mtandaoni Jijini Dar es Salaam, yakihusisha halmashauri 163 za Tanzania Bara na mikoa 12 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ushiriki wa wakuu wa mikoa hiyo na wataalam wao.
Nape alisema utekelezaji wa jambo hilo ni muhimu, kwani sekta ya mawasiliano ni wezeshi kwa sekta nyingine nchini.
“Mawasiliano ni sekta muhimu na mtambuka kwani sekta zote zinategemea mawasiliano ili zifanye kazi kwa ufanisi, zoezi la utekelezaji wa anwani za makazi ni jambo ambalo litawasaidia wananchi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kujiletea maendeleo,”alisema.
Waziri Nape alisema utekelezaji ni jambo muhimu ambapo Tanzania inatekeleza mfumo huo kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 – 2025, Ibara ya 61 (m) pamoja na miongozo ya Umoja wa Posta Afrika na Umoja wa Posta Duniani ambapo Tanzania ni nchi mwanachama.
Alisema utekelezaji wa mfumo huo ni moja kati ya mikakati ya kuiweka nchi katika mfumo wa kidijitali ili kurahishisha upatikanani wa huduma kwa wananchi pamoja na kurahisisha biashara ya mtandaoni ambapo serikali imedhamiria kuacha alama.
“Mradi huu ni moja ya miradi ambapo Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuacha alama na utekelezaji wake ulitakiwa ufanyike kwa miaka mitano lakini kwa sababu ya umuhimu wake mpaka mwezi Mei mwaka huu zoezi hili litakuwa limekamilika,”alisema.
Nape alisema utekelezaji wa anwani za makazi itakuwa ni zoezi ambalo litarahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambayo itafanyika Agosti mwaka huu na itakuwa rahisi kwa sababu ya upatikanaji wa anwani za makazi.
Katika hatua nyingine mafunzo hayo yalifunguliwa kwa mkoa wa Dar es Salaam ambapo Waziri Nape aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwaelimisha wananchi kwani ndiyo wanaviongozi wengi katika mitaa mbalimbali nchini.

Waziri Nape alieleza jinsi mkoa wa Dar es Salaam unahitaji utekelezaji wa haraka wa utambuzi na uwekaji wa anwani za mitaa pamoja na nyumba ambapo kata 46 kati ya 102 ndizo zoezi hilo limetekezwa lakini kwa ujumla majina 85,728 ya barabara yanahitajika na vibao milioni moja vya nyumba vinahitajika ili kazi hiyo ikamilike.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Jim Yonazi, alisema mfumo wa anwani ya makazi ni muhimu kwa wananchi.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amour Bakari, alisema kwa upande wao lilianza katika meneo manne ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri.
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, alisema mfumo huo wa anwani za makazi utakavyorahisisha biashara mtandao ambapo kwa sasa Shirika la Posta lina Jumla ya maduka 600 kupitia duka lake Mtandao ambayo kwa uhakika yanategemea upatikanaji wa anwani za makazi katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amoss Makala, alisema wapo tayari kutekeleza mradi huo, kwani umekuja muda mwafaka na wapo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mipango Miji ambao unalenga kuliboresha Jiji la Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu