WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameonya tabia inayofanywa na baadhi ya vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu hapa nchini ya kutuma maombi ya udahili na kudahili kwa niaba ya waombaji na kuwadhibitia (Confirmation) kitendo ambacho kinawanyima waomba Uhuru wa kuchagua vyuo wanavyovipenda.
Kufuatia vitendo hivyo Profesa. Ndalichako ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu kuchukua hatua stahiki kwa yeyote, Vyuo, Taasisi au mtu binafsi anayekiuka taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa uendeshaji katika eneo hilo.
Profesa. Ndalichako ametoa maelekezo hayo, wakati akifungua Mkutano wa kubadilishana uzoefu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa vyuo hivyo ili kufikia lengo hilo jijini Dar Es Salaam.
Waziri amesema kumekuwepo na vyuo vya elimu ya juu nchini,Taasisi au mtu binafsi kukiuka taratibu na kufanya usahili kwa niaba ya waombaji jambo ambalo ni kosa.

Amesema hiyo inawanyima waombaji uhuru binafsi wa kuchagua vyuo wanavyovitaka au wanavyoprnda kwenda kusoma, lazima TCU ichukue hatua staki kwa kila atakayebainika kufanya hivyo.
“Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wazara ya elimu kupitia TCU ni kosa kwa vyuo, taasisi kuwasajilia vyuo wanafunzi, wanaifanya vitenda hivyo nawasii waache mara moja, na naelekeza watakaobainika kuchukuliwa hatua stahiki,”amesisitiza Profesa. Joyce.
Katika hatua nyingine waziri huyo amewataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki nchini kusimamia kikamilifu uendeshaji wa Vyuo vyao ili kuhakikisha wanapunguza changamoto zilizopo.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upungufu wa wahadhiri wenye sifa stahiki, kutolipa wafanyakazi mishahara na stahiki nyingine, kuwepo kwa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia isiyokidhi viwango pamoja na ucheleweshaji wa matokeo ya mitihani.
“Kuna baadhi ya vyuo haviwalipi wafanyakazi hadi inapelekea wao kushikilia karatasi za mitihani ya wanafunzi na hivyo kuwanyima wanafunzi haki ya kupata matokeo yao kwa wakati. Hii si sawa kwa kuwa tunakuwa tunawaandaa wahitimu ambao wanatoka chuoni wakiwa na hasira na hivyo baadae kupata watendaji wasio na maadili bora,” amesisitiza Waziri Profesa.
Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo nafuu wa zaidi ya Sh.bilioni 972 kutoka Benki ya Dunia utakaotumika kuimarisha Elimu ya Juu ambapo jumla ya Vyuo 14 vitanufaika na kupunguza changamoto ikiwemo ya miundombinu.
Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe, alisisitiza umuhimu wa Menejinenti za Vyuo Vikuu kusikiliza na kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wanafunzi vyuoni badala ya kuyapuuza na hatimaye malalamiko hayo kuletwa Wizarani, vipo baadhi ya Vyuo ambavyo huchelewa kuwapa wanafunzi fedha za mikopo na kuwataka kuteua maafisa mikopo wenye uwezo ili kupunguza malalamiko hayo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Profesa.Lugano Kusiluka amekiri kupokea ushauri na maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi na kupunguza malalamiko na changamoto zilizopo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma