WAHITIMU wa mafunzo ya ndoa wametakiwa kuitumia elimu ya ndoa ipasavyo kwa kujenga subira na uvumilivu, ili kudumisha ndoa zao na kuepusha talaka zisizo na msingi, ambazo madhara yake huja kwa watoto.
Imeelezwa kuwa, ndoa nyingi huvunjika kwa kukosa maelewano na uvumilivu, hali inayosababishwa na wanandoa kutofuata yale wanayofundishwa kabla ya kuingia katika ndoa, jambo ambalo husababisha athari kubwa kwa watoto ambao huishia mitaani.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo, katika ukumbi wa msikiti wa Jaamiu Zinjibar Mazizini, wakati akikabidhi vyeti kwa wahitimu wa mkupuo wa kumi wa mafunzo ya ndoa.
Alisema lengo mafunzo hayo kwa wanandoa ni kuwafanya kuwa wavumilivu na kudumisha ndoa zao na kuwa walimu kwa wengine na kujenga imani subira na uvumilivu katika ndoa zao.
“Dawa pekee ya kudumisha ndoa ni kuwa na subira hususan kwa wanaume, ingawa changamoto kubwa ni wanawake kukosa uvumilivu katika ndoa,” alisema.
Aidha, alisema dini ya Kiislamu imetoa miongozo mbalimbali ya kisheria kwa lengo ya kuitunza ndoa na kuipa hadhi na heshima yake kwa kubainisha haki na wajibu kwa wanandoa.
Naye, Katibu wa Mufti Khalid Ali Mfaume, alisema aliridhishwa na mwamko wa wanafunzi wanaohitaji elimu ya ndoa, jambo ambalo litasaidia kuepusha wimbi la talaka nchini.
Alisema mafunzo mbalimbali waliyoyapata wahitimu hao ni maana ya ndoa kisheria, uchaguzi wa mchumba katika uislamu nafasi ya wazazi kwa wanandoa na sifa za familia ya Kiislamu na viashiria vya migogoro katika ndoa na matokeo ya migogoro hiyo.
Mafunzo hayo ya mkupuo wa kumi yalifanyika kwa wiki kumi na kujumuisha wanafunzi 195 wa kike na kiume .