SERIKALI imetangaza mikakati ya kukabiliana na ongezeko la bei ya mbolea, uhaba wa mafuta ya kula na sukari nchini.
Imesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, inatarajia kutumia sh. bilioni 150 kutoa ruzuku ya mbolea kwa mazao yote.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Kilimo Bungeni Dodoma, Waziri wa wizara hiyo, Hussein Bashe, alisema utaratibu wa ruzuku hiyo utaelezwa wakati wa uwasilishwaji wa Bajeti Kuu ya Serikali.
“Ruzuku hiyo haitakuwa ya kudumu, bali itatolewa kwa kipindi maalumu hususan wakati yatapotokea majanga au mdororo wa kiuchumi,” alisema Bashe.
UPUNGUFU WA MAFUTA
Akizungumzia mkakati wa kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula, alisema wizara imejiwekea lengo la kuzalisha tani milioni tatu za alizeti ifikapo mwaka 2025, ambapo ili nchi iwe na mafuta tani milioni moja inahitajika kulimwa eneo lenye ukubwa wa hekta milioni 2.4.
Bashe alisema ili kufikia lengo, katika mwaka 2022/2023 serikali itachukua hatua mbili za kimkakati moja wapo ni kuzalisha na kugawa tani 5,000 za mbegu bora za alizeti kwa ruzuku, ambapo sh. bilioni 11 zitatumika kuzalisha mbegu hizo.
“Katika mwaka 2023/2024, wizara itagawa tani 10,000 na mwaka 2024/2025 itazalisha na kugawa tani 15,000 za mbegu bora za alizeti. Shughuli ya uzalishaji wa mbegu itafanywa na ASA na kuingia mikataba na kampuni binafsi kuzalisha mbegu ambazo zitagawiwa kwa wakulima kwa ruzuku.
Alisisitiza kuwa: “Hatua ya pili, wizara inajadiliana na Wizara ya Fedha na Mipango kuweka motisha ya kikodi kwa viwanda vinavyozalisha mafuta ya alizeti nchini kwa kuwaondolea kodi ya ongezeko la thamani (VAT).’
UHABA WA SUKARI
Kuhusu upungufu wa sukari nchini, alisema wizara kupitia Bodi ya Sukari itaongeza uzalishaji kutoka tani 372,210 mwaka 2021/2022 hadi tani 450,000 mwaka 2022/2023.
Alieleza lengo hilo litafikiwa kwa kutekeleza mipango ya muda mfupi ya kuimarisha udhibiti wa visumbufu, kuimarisha upatikanaji wa maji shambani na kupunguza upotevu wa miwa kwa kuhakikisha viwanda vinafanya kazi kwa ufanisi.
“Mipango hiyo itaenda pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa sukari ya viwandani. Aidha, mipango ya muda wa kati ni kusimamia upanuzi wa viwanda vya sukari vya Kilombero, Kagera na Mtibwa ili kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 372,210 hadi tani 635,012 mwaka 2025/2026,” alisisitiza.
Bashe ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alibainisha ongezeko hilo litatokana na kuongeza uzalishaji wa miwa kutoka tani 800,000 hadi tani 1,700,000 kwa wakulima wadogo wa mashamba ya Kilombero, upanuzi wa mashamba ya miwa ya Kagera na Mtibwa yenye ukubwa wa hekta 13,000 na 30,000.
Pia, alisema kazi hiyo itaimarisha miundombinu ya umwagiliaji ukiwemo ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji ya umwagiliaji lenye mita za ujazo 25,000,000 katika mashamba ya Mtibwa.
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA