SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imevitaka vyombo vya sheria kujipanga na kufanya kazi kwa kushirikiana katika utekelezaji wa sheria mpya ya kuundwa kwa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kuhakikisha watuhumiwa wanatia hatiani na kesi zinasikilizwa kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, alipofanya mazungumzo na uongozi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ukiongozwa na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Shaaban.
Mazungumzo yalihusu utekelezaji wa sheria mpya ya Mamlaka ya Kupambana na Dawa ya Kulevya yaliyofanyika Migombani, Unguja.
Amesema uwepo wa sheria kamili ya kuundwa kwa mamlaka hiyo itasaidia na kurahisisha kazi ya kutokomeza dawa hizo na kuondokana na urasimu uliokuwepo awali ambao ulikuwa kikwazo kikubwa katika mapambano hayo.
Dk. Saada alivitaka vyombo vya sheria kujipanga zaidi katika kuhakikisha azma ya serikali ya kupambana na dawa hizo inafikiwa kikamilifu na hatimaye kushinda vita hivyo.
Waziri huyo alisema muswaada wa kuundwa kwa mamlaka kamili ya kupambana na dawa hizo umeungwa mkono na wajumbe wa baraza la wawakilishi ambao wameonyesha utayari wa kupambana na suala hilo.
”Matarajio makubwa ya serikali baada ya kupitishwa muswaada wa kuundwa kwa mamlaka kamili ya Kupambana na Dawa za Kulevya ni kuanza kwa utekelezaji wake ambapo tunahitaji ushirikiano mkubwa wa vyombo vya sheria ambavyo vina uzoefu mkubwa katika kuendesha na kusimamia mwenendo wa kesi mahakamani,”alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Shaaban, amesema wamejipanga kuhakikisha wanaitumia sheria mpya ya kuundwa kwa mamlaka hiyo na kwenda na kasi ya kusikiliza kesi za watuhumiwa kwa haraka.
Amesema tayari Ofisi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar imekamilisha kazi ya kuteua majaji watakaosimamia kesi za dawa za kulevya haraka kwa kuzipatia hukumu yake.
Kaimu Jaji Mkuu huyo ametaka kuwepo kwa ushirikiano kwa baadhi ya taasisi za sheria likiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika kuharakisha mwenendo wa mashtaka na kutoa hukumu.
”Mahakama Kuu ya Zanzibar tayari tumejipanga vizuri kuhakikisha kesi za tuhuma za dawaza kulevya zinasikilizwa haraka na kutolewa hukumu kwa sababu ipo mamlaka kamili inayoshughulikia masuala hayo kuanzia kukamata,kufanya upelelezi na kufikisha mahakamani,”alisema.
Naye, Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Isaya Kayange, alisisitiza ushirikiano wa pamoja ambapo wananchi wawe tayari kutoa ushahidi mbele ya mahakama ambao ndiyo utakaowatia hatiani watuhumiwa hao.
Na Khatib Suleiman, Zanzibar