WABUNGE sita wamejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Unaibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo vigogo wawili ambao ni Mbunge wa Ilala Mussa Zungu na Mbunge wa Nzega Vijijini Khamis Kigwangala.
Wengine ni Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile, Mbunge wa Mahonda, Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa Hanang’, Mhandisi Samwel Hhayuma na Mbunge wa Muleba Kusini, Dk. Oscar Kikoyo.
Hatua ya uchukuaji fomu ya kugombea nafasi ya Naibu Spika imekuja kutokana na Januari 31 Mwaka huu aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mbunge wa Mahonda mkoa wa kaskazini Unguja, Abdullah Ali Mwinyi amesema anaimani anaweza kuitumikia nafasi ya unaibu Spika iwapo chama Cha Mapinduzi kitampitisha kugombea nafasi ya unaibu Spika.
Mwinyi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa awamu ya 2 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni mdogo wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ally Mwinyi.
Mwinyi amebainisha kuwa ameamua kuchukua fomu kwakuwa ana uwezo wa kuitumikia nafasi hiyo kwani uzoefu anao na amekua Mbunge kwa vipindi 3 tofauti ambapo mara mbili amekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mimi ni Mwanasheria mzoezfu ninaimani ninauwezo wa kuitumikia nafasi ya unaibu Spika kwa kutumia utulivu,hekima na maarifa,”amesema Mwinyi.
Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Ilala Mussa Zungu amesema ameamua kuchukua fomu kwa sababu kiti kipo wazi na ana sifa kwakuwa sifa ya mgombea lazima awe Mbunge.
“Nikipata nafasi nitapokea maelekezo kutoka kwa Spika na kutimiza majukumu nitakayoelekezwa kwa asilimia 100 kama Msaidizi wake,” amesema Zungu.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu 5 Dkt. Hamis Kigwangalla, ameeleza amechukua fomu kwa sababu ana sifa zote kwa mujibu wa katiba ya nchi na ya Chama Cha Mapinduzi na kanuni za uchaguzi ndani ya chama.
“Ninajiamini sababu nina uzoefu wa kutosha kama Mbunge maana nina uwezo wa kusimamia wabunge na kuishauri Serikali kwakuwa nina uzoefu wa kutosha,”amesema.
Kwa upande wa Mbunge wa Hanang’ Mhandisi Samwel Hhayuma ameeleza kuwa ameamua kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kwa sababu nafasi hiyo ipo wazi na sifa anayo.
Amesema ikiwa atapata ridhaa ya kuongoza kiti hicho ataisimamia Serikali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapundizi kwa kuwa yeye ni daraja kati ya wananchi na Serikali.
Februari 4, mwaka huu, Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alitangaza ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo kupitia chama hicho.
Kupitia taarifa hiyo Shaka ameeleza kuwa, wagombea wanatakiwa kuchua fomu na kuzirejesha kuanzia Feb 4-6,2022 kuanzia asubuhi hadi saa tisa alasiri huku Feb 7,2022 ikiwa ni siku ambayo Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM itakaa kujadili wagombea na kuishauri kamati kuu ya CCM Taifa.
Amesema Februari 8,2022 kutakuwa na tukio la Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ambapo Februari 10, 2022 Kamati ya wabunge wa chama hicho itapiga kura kupitisha jina la Naibu Spika.
NA SELINA MATHEW, DODOMA